Ujenzi wa barabara hapa nchini umepigwa jeki na tangazo la Rais William Ruto kwamba wanakandarasi wa ujenzi wa barabara watalipwa shilingi bilioni 20 kuanzia juma lijalo.
Kulingana na kiongozi wa taifa, utoaji wa fedha hizo unalenga kuhakikisha ujenzi wa barabara hautatizwi kote nchini.
Tangazo hilo la Rais Ruto linajiri mwezi mmoja baada ya serikali kukamilisha malipo ya shilingi bilioni 177 kwa wanakandarasi wa barabara.
Akizungumza katika kanisa la Africa Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA) Mahiga, eneo bunge la Othaya Constituency, kaunti ya Nyeri, Rais Ruto alisema kaunti hiyo imetengewa shilingi bilioni nane kwa upanuzi wa barabara katika maeneo bunge yake yote.
“Uwekaji lami wa barabara ya Mau Mau roads, ambao ulikuwa umekwama, sasa unaendelea, huku barabara zingine zikiimarishwa kufanikisha uchukuzi wa bidhaa na huduma zingine,” alisema Rais Ruto.
Aidha, kiongozi wa taifa alidokeza kuwa ujenzi wa barabara ya safu mbili ya Kenol-Marua dual, inayounganisha kaunti za Murang’a, Kirinyaga na Nyeri, sasa imekamalika kwa asilimia 90, kutoka asilimia 30 mwaka 2022.
“Itakapokamilisha, barabara hiyo ya safu mbili itapanuliwa kufika Nyeri mjini hasi Nanyuki,” aliongeza Rais Ruto.