Uganda yajinadi kwenye mabasi Italia

Inatekeleza kampeni ya kutangaza Uganda kama eneo zuri la Utalii.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali ya Uganda imeanzisha mpango mpya wa kujitangaza kama eneo zuri la kitalii nchini Italia.

Inafanya hivyo kupitia mabango ya picha za maeneo mbali mbali ya taifa hilo la Afrika Mashariki kwenye mabasi ya abiria ya Italia.

Kampeni hiyo ambayo lengo lake la msingi ni kuvutia watalii zaidi wa kimataifa nchini Uganda ilizinduliwa na Balozi wa Uganda jijini Roma, Elizabeth Paula Napeyok.

Picha wanazoonyesha kwenye mabasi ya Italia ni pamoja na za wanyama wanaopatikana kwenye mbuga za Uganda kama sokwe wa milimani na korongo taji, ambao wamekuwa nembo za taifa hilo kwa miaka mingi.

Mabasi ya uchukuzi wa abiria yanayohusika kwenye matangazo hayo ni yale yanayopitia maeneo muhimu ya Italia kama Roma, Milan, Venice na Florence.

Akitangaza mwanzo wa shughuli hiyo, Balozi Napeyok alidhihirisha imani kwamba picha hizo zitavutia raia wa Italia na wageni wanaozuru Italia ili wawazie kufanya Uganda kuwa eneo lao lijalo la utalii.

Napeyok anatizamia kwamba kampeni hiyo kwenye barabara za Italia itafikia watu wapatao Milioni 10 na wengi kati yao anaamini watafika Uganda.

Mataifa mengi ya Afrika hutegemea pakubwa utalii kama njia ya kujipatia mapato.

Share This Article