Chama cha ODM leo Ijumaa kinaandaa Mkutano Maalum wa Wajumbe wa chama hicho (SDC).
Mkutano huo unafanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Nairobi.
Kwenye mkutano huo, Dkt. Oburu Oginga ameidhinishwa kuwa kiongozi wa chama hicho huku Magavana Simba Arati wa Kisii na Abdullswamad Sheriff Nassir wa Mombasa wakiidhinishwa kuwa naibu wake.
Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga ataendelea kuhudumu kama mwenyekiti wa chama.
Awali, chama hicho kilitangaza kuwa hakutakuwa na uchaguzi wa uongozi wala marekebisho ya katiba ya chama wakati wa mkutano huo.
Hata hivyo, haikujulikana ikiwa msimamo huo utadumishwa baada ya uamuzi wa hiyo jana wa jopo la kusuluhisha mizozo ya vyama vya kisiasa.
Jopo hilo lilielekeza kuwa mifumo ya ndani chamani itumiwe kwanza kusuluhisha mivutano kati ya wanachama wakati Katibu Mkuu wa sasa Edwin Sifuna akiendelea kuhudumu kwenye wadhifa huo.
Sifuna, ambaye pia ni Seneta wa Nairobi, alikuwa amevuliwa wadhifa huo na mwakilishi wa wanawake wa Busia Catherine Omanyo kutakiwa kuukaimu.
Mrengo wa chama hicho unaoongozwa na Sifuna na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino umekuwa uikishinikiza kufanywa kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa chama.
Wanasema kaimu kiongozi wa ODM Dkt. Oburu Oginga yuko ofisini kinyume cha sheria kwani hakuchaguliwa na wajumbe.
Ni hali ambayo imesababisha mivutano chamani, mrengo mmoja ukiunga mkono ndoa kati ya ODM na chama tawala cha UDA huku mwingine ukipinga.