Kituo cha KBC Redio Taifa kimetuzwa na Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania (BAKITA), kutokana na mchango wake katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili.
Kituo hicho kinachomilikiwa na Shirika la Utangazaji Nchini (KBC), kiliibuka mshindi baada ya kuvishinda vituo vingine kwenye kongamano la 5 la idhaa za kiswahili duniani lililoandaliwa Jijini Arusha, Tanzania.
Kongamano hilo limetajwa kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wanahabari, wataalamu wa lugha, watangazaji na wadau wa mawasiliano kutoka pembe mbalimbali za dunia.
Lengo kuu lake ni kukuza, kuendeleza na kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika vyombo vya habari kimataifa.
Wakati huo huo, mtangazaji wa Shirika la KBC Mathias Momanyi alipokea tuzo ya “Mwenezi Lugha Mahiri wa Kiswahili 2026”, kwenye kongamano hilo.
Katika kongamano hilo, tuzo mbalimbali zilitolewa kwa kutambua mchango bora katika kukuza Kiswahili kupitia vyombo vya habari. Tuzo hizo zilihusisha vipengele kama:
- Idhaa bora ya Kiswahili kimataifa
- Mtangazaji bora wa redio/televisheni
- Ubunifu katika matumizi ya Kiswahili kwenye majukwaa ya kidijitali
- Mchango wa kipekee katika kukuza lugha ya Kiswahili
Tuzo hizi zililenga kuhamasisha ubunifu, ushindani chanya na ubora katika tasnia ya uanahabari wa Kiswahili.
Wengine waliotuzwa ni pamoja na Mwajuma Mutoyi kutoka Burundi, Fay Shao kutoka Afrika Kusini na Radio Maria, DW, Radio – RFI Ufaransa, ZBC, CGTV, TBC miongoni mwa vituo vingi vya televisheni.
Jumla ya washiriki 943 na wawasilishaji 250 katika makala mbalimbali, ni miongoni mwa waliohudhuria kongamano hilo.