Serikali kujenga soko la kisasa Sori, kaunti ya Migori

Rais Ruto alisema hayo alipokamilisha ziara yake ya kimaendeleo huko Nyanza.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa katika mji wa Sori, kaunti ya Migori ili kuchochea biashara ya ndani.

Rais William Ruto alisema hayo katika siku yake ya tano na ya mwisho ya ziara ya maendeleo eneo la Luo Nyanza.

Alisema serikali yake pia imepata mwekezaji wa sekta binafsi atakayeanzisha kiwanda kipya cha kusaga mpunga huko Nyatike, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya ndani na kusaidia wakulima.

Kiongozi huyo wa nchi aliongeza kuwa mipango inaendelea ya kujenga bandari ndogo na kuendeleza maeneo ya kisasa ya kushushia samaki ili kufufua shughuli za uvuvi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, ikiwemo Sori.

Rais Ruto pia alizindua ujenzi wa mradi wa nyumba za gharama nafuu wa Sori wenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 wenye nyumba 748 katika eneo bunge la Nyatike, kaunti ya Migori.

Rais alisema uwekezaji huo unatarajiwa kubuni zaidi ya nafasi za kazi 10,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa vijana.

Share This Article