Chama cha ODM kimesema maandalizi yamepambana moto kuelekea mkutano wake maalum wa wajumbe (SDC) utakaoandaliwa Machi 27 mwaka huu.
Chama hicho kilitoa ilani ya mkutano huo Machi 6.
Akiwahutubia wanahabari akiwa ameandamana na viongozi wengine wa chama, Naibu Katibu Mkuu wa ODM Catherine Omanyo alisema mkutano huo utafanyika katika uwanja wa Jamhuri jijini Nairobi.
“Tangu kutolewa kwa ilani, tumeshiriki msururu wa shughuli mbalimbali kwa maandalizi ya siku hii ambayo ajenda yake iliwekwa katika NOTISI,” alisema Omanyo.
Chama hicho kikiweka bayana kuwa wakati wa mkutano huo, hakutakuwa na uchaguzi wa uongozi wala marekebisho ya katiba ya chama.
Mrengo wa chama hicho unaoongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino umekuwa uikishinikiza kufanywa kwa uchaguzi wa viongozi wapya wa chama.
Wanasema kaimu kiongozi wa ODM Dkt. Oburu Oginga yuko ofisini kinyume cha sheria kwani hakuchaguliwa na wajumbe.
Ni hali ambayo imesababisha mivutano chamani, mrengo mmoja ukiunga mkono ndoa kati ya ODM na chama tawala cha UDA huku mwingine ukipinga.
Awali, chama hicho kilikanusha madai ya kuchapishwa kwa ilani ya mkutano maalum wa wajumbe katika gazeti moja la humu nchini iliyodaiwa kutiwa saini na Dkt. Oginga kikiitaja kuwa bandia.