Rais William Ruto leo Alhamisi amezindua awamu ya 2B ya ujenzi wa reli ya SGR katika hafla iliyofanyika katika kaunti ya Narok.
Awamu ya 2B inahusisha ujenzi wa SGR kutoka mjini Naivasha hadi Kisumu.
Ruto keshokutwa Jumamosi mjini Kisumu anatarajiwa kuzindua awamu ya 2C inayohusisha ujenzi wa reli hiyo kutoka mji wa Kisumu hadi mji wa mpakani wa Malaba katika kaunti ya Busia.
Hafla ya leo ya uzinduzi wa 2B imefanyika katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Narok.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri Davis Chirchir wa Barabara na Uchukuzi na Opiyo Wandayi wa Nishati, na Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu miongoni mwa viongozi wengine.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Ruto alisema kuna umuhimu wa kujenga reli hiyo hadi kufika Kisumu, Busia na kisha nchi zingine za Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC ili kuhakikisha manufaa yake yanadhihirika wazi.
Kulingana naye, mradi huo utasaidia mno kupunguza gharama ya kufanya biashara na usafiri, na usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi za Afrika Mashariki.
Ruto aliongeza kuwa reli hiyo itasaidia kuifanya Kenya na jiji la Kisumu kuwa kituo kikuu cha biashara.
Viongozi mbalimbali waliozungumza walisifia mradi huo wakisema utasaidia kuboresha biashara, usafiri na kufungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo ambako reli hiyo itapita.
Mudavadi alitaja uzinduzi huo kuwa siku kubwa zaidi, kwani utasaidia kuimarisha uchumi wa taifa hili kwa kiwango kikubwa.

Aliongeza kuwa mradi huo pia utakuwa na manufaa mengi kwa wakazi wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kubuni nafasi za ajira na kuboresha biashara.
Alielezea imani kuwa ingawa mradi huo ni wa gharama kubwa, manufaa yake yatadhihirika punde ujenzi wake utakapokamilika.

Awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa reli ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi na kisha Nairobi hadi Naivasha.