Edrisah Kenzo Musuuzah, mwanamuziki wa Uganda ambaye wengi wanamfahamu kama Eddy Kenzo, amefurahikia sheria mpya ya hakimiliki nchini Uganda akisema ni zaidi ya mchakato wa kisheria.
Haya yanafuatia kupitishwa bungeni kwa mswada wa marekebisho ya sheria kuhusu hakimiliki na haki husika wa mwaka 2025 na Kenzo anahisi sasa kwamba muziki wa Uganda una thamani.
Akizungumza kwenye mahojiano, Kenzo ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais kuhusu wabunifu, alisema kwamba mapambano kuhusu hakimiliki hayakuwa tu kuhusu pesa.
Nyota huyo wa muziki alisema kwamba sheria hiyo mpya ni hakikisho kwake na kwa wanamuziki wengine kwamba kazi zao zinabeba thamani halisi.
Kenzo alizungumza kuhusu jinsi wasanii wameumia kwa miaka mingi wakiona kazi zao zikiletea watu wengine mapato huku wapo wakipata pesa kidogo au kukosa kabisa.
Mwimbaji huyo alisema ametekeleza wajibu wake kama mwanamuziki na alifika bungeni kwa sababu ya shida zinazokabili tasnia ya muziki nchini Uganda.
Kulingana naye, wasanii wengi hujawa na woga kila siku kuhusu maisha yao ya baadaye hasa wakati ambapo umaarufu wao utadidimia.
“Siwezi kuwa katika tasnia ambayo nikizeeka, wanangu wataniona kama mtu wa mchezo tu,” alisema Kenzo akiongeza kwamba kwa sasa wasanii wana nguvu ya kutumbuiza jukwaani lakini katika muda wa miaka kadhaa watakosa hizo nguvu.
Wasanii nchini humo sasa wana matumaini kwamba sheria hii mpya itabadilisha mambo kwa kulinda kazi zao na kuboresha jinsi mirahaba inakusanywa na kusambazwa.