Mudavadi: Raia wa Kenya hawatasajiliwa kwenye majeshi ya kigeni

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri Mwenye Mamlaka Makuu, aliypia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, akiwa Moscow, Russia.

Waziri Mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ametangaza kuwa raia wa Kenya hawatajumuishwa katika Vikosi vya Ulinzi vya Russia, kufuatia makubaliano yaliyofanywa Jijini Moscow Jumatatu.

Mudavadi aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje, alidokeza kuwa mikakati imewekwa kuwasaidia Wakenya wanaohitaji usaidizi wa aina yoyote, kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa wanahabari na mwenzake wa Russia Sergey Lavrov Jijini Moscow, Mudavadi alisema swala hilo limejadiliwa kupitia njia za kidiplomasia kati ya Kenya na Russia.

Alisema serikali ya Russia imekubali kurejesha nchini Kenya miili ya Wakenya waliofariki, ikiwa kutapatikana safari za ndege za moja kwa moja kati ya Russia na Kenya.

Wizara ya Mambo ya Nje inakadiria kuwa takriban raia 252 wa Kenya walijiunga na Vikosi vya Ulinzi vya Russia wakiwemo maafisa wa zamani wa Jeshi la ulinzi la Kenya, Huduma ya Taifa ya polisi, Huduma ya Vijana kwa Taifa na Huduma ya Magereza.

Hadi kufikia sasa raia 44 wamerejea nyumbani, 38 wamelazwa hospitalini, 10 wamefariki au kutoweka na 160 wangali katika vikosi hivyo.

Mudavadi yuko nchini Russia kwa ziara rasmi ya kiserikali, itakayokamilika Machi 18, 2026.

Share This Article