Tonto Dikeh, mwigizaji, mwanasiasa na mhubiri wa Nigeria amejipata pabaya kutokana na alichokifanya katika shule moja nchini humo.
Dikeh amekuwa akitangaza mipango ya usaidizi ambayo amekuwa akitekeleza katika shule mbali mbali nchini Nigeria ambapo amekuwa akiwalipia wanafunzi ada za mtihani wa kitaifa.
Kupitia akaunti yake ya Instagram, Tontoh alieleza kwamba alitakiwa kuchagua kati ya eneo la makahaba, hospitali na shule katika mpango wake wa mahubiri na akaamua kuchagua shule.
Alichapisha picha na video za ziara yake katika shule husika ambapo alionekana akimwombea mwanafunzi mmoja wa kike aliyekuwa amebanwa chini ardhini huku wengi wakihisi kwamba mtoto huyo alikuwa akiumizwa.
Tonto anaonekana akiwa ameshikilia kichwa cha mtoto huyo vidole vyake vikiwa vinafinya macho ya mtoto husika ambaye alikuwa analia huku Tonto na wenzake wakisikika wakiomba.
Mkosoaji wa mitandaoni nchini Nigeria Very Dark Man almaarufu VDM amechapisha video ya kumkanya Tonto kutokana na tendo hilo.
VDM anadai kwamba shule husika ni ya nyumbani kwao na kamwe hawezi kukubali watoto kupotoshwa kidini.
Alisema Tonto mwenyewe amejaribu uigizaji, akafanyiwa upasuaji wa kuongeza makalio, akaingilia siasa na sasa Mungu amemwokoa.
VDM alimhimiza Tonto kubadilisha maisha ya watoto hao kwa namna nyingine na wala sio kwa kuwahubiria tu na kuwaombea akishangaa alikuwa anamtoa mtoto huyo mapepo gani.
Doris Ogala kwa upande wake amewataka maafisa wa polisi kuingilia kati na kumkomesha Tonto Dikeh kwani kulingana naye, alikuwa tu akifanya majaribio ya kutoa watu mapepo na akachagua kufanyia watoto bila hata idhini ya wazazi wao.