Serikali imetoa shilingi bilioni moja kwa ujenzi wa soko la kisasa katika eneo la Gakoromone, kaunti ya Meru.
Akithibitisha hayo siku ya Jumatatu, Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki alisema serikali kuu pia inatekeleza miradi mingine ya maendeleo katika eneo hilo.
Miradi hiyo ni pamoja na kuboresha hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Meru kwa kitita cha shilingi bilioni moja, ujenzi wa barabara Meru Mjini utakaogharimu shilingi bilioni 3.7 na mradi wa kukamilisha ujenzi wa uwanja wa Kinoru utakaogharimu shilingi milioni 900.
“Miradi ya ujenzi wa barabara inaendelea katika maeneo bunge yote 9 katika kaunti ya Meru, kwa kitita cha shilingi bilioni 39. Masoko mengine 19 yanajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni mbili, huku mradi wa uunganishaji umeme katika eneo hilo ukigharimu shilingi bilioni 2.3,” alisema Prof. Kindiki.
Aliyasema hayo alipokuwa akiwahamasisha wananchi kuhusu ujenzi wa soko la Gakoromone, pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na serikali kuu.
Kwenye mkutano huo, Prof. Kindiki aliandamana na Gavana wa Meru Isaac Mutuma, Naibu Gavana Linda Kiome, mwakilishi wa wanawake Elizabeth Kailemia, wabunge Rahim Dawood (Imenti Kaskazini), Mpuru Aburi (Tigania Mashariki), Dan Kiili (Igembe ya Kati ), Dorothy Muthoni (Mbunge Mteule ), Wawakilishi wadi na viongozi wengine.