Gavana Arati: Mashemeji walinilipia tikiti za MCAs

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kisii Simba Arati amefafanua kwamba wawakilishi wadi ambao alisafiri nao hadi Uchina mwezi jana, walilipiwa tikiti za ndege na serikali ya nchi hiyo.

Simba alikuwa akizungumza kwenye hafla ya ibada inayoendelea katika uwanja wa nyanturago huko Nyaribari Chache kaunti ya Kisii inayohudhuriwa na Rais William Ruto.

Matamshi yake yanafuatia tetesi ambazo zimesheheni midomo ya wengi katika kaunti ya Kisii , wengi wakidai kwamba alitumia pesa za serikali ya kaunti visivyo kwa kusafirisha wawakilishi wadi wapatao 50 hadi Uchina kwa ziara ya kujifahamisha.

“Ndio nilienda na MCAs 50 kule Uchina, lakini sikutumia pesa ya umma hata shilingi moja! Wale ma-inlaw waliweza kunipea ticket za wa-MCA 71.” alielezea Simba akisema wale ambao hawakusafiri naye hawakubaguliwa bali wengi wao hawakuwa na paspoti na wengine hawawezi kusafiri kwa ndege kwa sababu za kiafya.

Anarejelea watu wa Uchina kama mashemeji kwani mke wake ni mzaliwa wa huko.

Kuhusu ushirikiano na serikali kuu, Simba alisema yuko tayari kufanya kazi na Rais kwa manufaa ya watu wa kaunti ya Kisii.

Alimwomba Rais asaidie katika kujenga uwanja wa michezo wa Nyanturago ambao wanatumia kwa hafla ya leo.

Simba Arati na mshindani wake mkuu kisiasa Sylvanus Osoro ambaye ni mbunge wa Mugirango Kusini walipigana pambaja hadharani Osoro alipomkaribisha kuzungumza hatua ambayo ilishangiliwa na wakazi wa kaunti ya Kisii wanaohudhuria hafla hiyo.

Website |  + posts
Share This Article