Naibu Karani na aliyekuwa Spika wa bunge la Kisii wakamatwa kwa ufisadi

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wawili wa Kaunti ya Kisii wakamatwa kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC, imewakamata Naibu Karani na Spika wa zamani wa bunge la kaunti ya Kisii, kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Daniel Mbaka Omwoyo na David Ondimu Kombo, wanadaiwa kuwaajiri wafanyakazi wa bunge hilo kinyume cha sheria.

Kupitia ukurasa wa X leo Jumanne, EACC ilisema baada ya uchunguzi ilibainisha kuwa Omwoyo alimwajiri mpwa  wake Everline Maraburi kinyume cha sheria katika bunge la kaunti hiyo, bila kuzingatia utaratibu wa bodi ya Utumishi wa Umma ya kaunti hiyo.

Kulingana na EACC, Maraburi alipewa jukumu la msaidizi wa kibinafsi wa Spika kwa masharti ya kudumu kinyume na sheria za Tume ya kuratibu Mishahara na Marupurupu, zinazomruhusu Spika kuwateua baadhi ya wafanyakazi akiwemo msaidizi wa kibinafsi.

Kwa upande wake, aliyekuwa spika wa zamani, alichukuliwa hatua kwa kuruhusu uteuzi wa Maraburi alipokuwa mamlakani.

Omwoyo alifikishwa katika mahakama moja ya Kisii na kukanusha madai hayo, huku akiachiliwa kwa dhamana ya shilingi 50,000 pesa taslimu.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article