Uhispania imejikatia tiketi ya kwota fainali ya Kombe la Dunia kwa wanawake kwa mara ya kwanza,baada ya kuichachafya Uswizi mabao 5 kwa moja katika mchuano wa raundi ya 16 bora uliosakatwa ugani Eden Park nchini New Zealand mapema Jumamosi.
Mshambulizi Aitana Bonmati alifungua karamu ya magoli kwa Uhispania kunako dakika ya 5 kabla ya beki Lala Codina kujifunga dakika ya 11.
Redondo Ferrer aliwarejesha Waspanyola uongozini dakika ya 17 kabla ya Bonmati na Codina kuongeza moja kila mmoja dakika ya 36 na 45 mtawalia huku kipindi cha kwanza kikimalizika kwa uongozi wa Uhispania wa magoli manne kwa moja.
Jennifer Hermoso alitikisa nyavu kwa bao la pekee la kipindi cha pili kukamilisha ushindi maridhawa wa Uhispania.
Uhispania watachuana na mshindi kati ya Uholanzi na Afrika Kusini kwenye robo fainali.