Takriban watu sita wanahofiwa kufariki na wengine tisa kujeruhiwa, baada ya nyambizi ya watalii kuzama katika ufuo wa mji wa Hurghada wa Bahari ya Shamu mapema Alhamisi.
Inaaminika kuwa takriban abiria 40 ambao ni watalii walikuwa kwenye nyambizi hiyo, ajali hiyo ilipotokea.
Ubalozi wa Urusi nchini Misri, umesema kuwa watalii wote waliokuwa kwenye meli hiyo walikuwa raia wa Urusi.
Katika chapisho kwenye ukurasa wa Facebook, ubalozi huo umesema kwamba abiria 45 walikuwa kwenye chombo hicho, wakiwemo watoto.
Chapisho hilo linaongeza kuwa bado wanasubiri taarifa zaidi kuhusu abiria wengine kadhaa.
Tukio hilo lilitokea mwendo wa saa 10:00 kwa saa za Misri, karibu kilomita moja kutoka ufukweni, kulingana na duru za kuaminika.