Kenya kutuma mjumbe maalum kusuluhisha mzozo nchini Sudan Kusini

Martin Mwanje
3 Min Read
Rais William Ruto

Rais William Ruto amefanya mazungumzo na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir kufuatia mzozo unaotokota nchini humo na uliosababisha kukamatwa na kuzuiliwa nyumbani kwake kwa Makamu wa Rais wa kwanza wa nchi hiyo Dkt. Riek Machar jana Jumatano.

Ruto anasema Kenya itatuma mjumbe maalum Sudan Kusini ili kusaidia kutuliza mzozo unaoshuhudiwa nchini humo kwa sasa.

Kwenye ujumbe katika mtandao wake wa X, Rais Ruto ambaye pia ni mwenyekti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema amechukua hatua hiyo baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

“Nimefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Salva Kiir juu ya hali iliyosababisha kukamatwa na kuzuiliwa kwa Makamu wa Rais wa kwanza Riek Machar nchini Sudan Kusini,” amesema Rais Ruto.

“Baada ya mashauriano na Rais Museveni na Waziri Mkuu Abiy, ninatuma mjumbe maalum nchini Sudan Kusini kufanya mashauriano, kujaribu kusuluhisha mzozo huo na kututaarifu yaliyoafikiwa.”

Awali, Kenya ilielezea mashaka kuhusiana na hali ilivyo nchini Sudan Kusini, hasa kutokana na ripoti kwamba Dkt. Machar alizuiliwa nyumbani kwake jana Jumatano usiku.

Kwenye taarifa, Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi alitoa wito kwa pande husika katika mzozo unaorindima nchini humo kuwa mstari wa mbele kutafuta amani ya kudumu.

“Serikali ya Kenya inatoa wito kwa pande zote nchini Sudan Kusini kutoa kipaumbele nchini humo kwa kutoa nafasi kwa makubaliano ya amani yanayoendelea chini ya mwavuli wa Makubaliano ya Uhuishaji ya IGAD juu ya Utatuzi wa Mgogoro katika Jamhuri ya Sudan Kusini (R-ARCSS),” alisema Mudavadi kwenye taarifa iliyotolewa leo Alhamisi.

“Tunatoa wito kwa viongozi wote wa Sudan Kusini kujizuia mno, kusitisha uhasama, na kuheshimu Makubaliano ya Amani Yaliyohuishwa kwa maslahi bora ya mamilioni ya watu wao,” aliongeza Mudavadi ambaye pia ni Mkuu wa Mawaziri.

Taarifa za kukamatwa na kuzuiliwa kwa Dkt. Machar nyumbani kwake zilitolewa na chama chake cha Sudan People’s Liberation Movement (SPLM/IO).

Kiliongeza kuwa msafara wenye silaha ukiongozwa na maafisa wakuu wa usalama uliingia katika makazi ya Dkt. Machar katika mji mkuu, Juba, na kuwanyang’anya walinzi wake.

Dkt. Machar ni mpinzani wa muda mrefu wa Rais wa nchi hiyo Salva Kiir.

 

Website |  + posts
Share This Article