Serikali kutumia michezo kupiga jeki utalii

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Utalii na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei wakijumuika na watumbuizaji, Nyahururu. Picha na Lydia Mwangi.

Serikali inalenga kutumia michezo kupiga jeki sekta ya utalii hapa nchini, kwa mujibu wa Waziri wa Utalii Rebecca Miano.

Waziri Miano amesema mashindano ya uendeshaji baiskeli hasa katika vivutio vya utalii ni muhimu katika kupigia debe vivutio vya kitalii katika eneo la Bonde la Ufa.

Miano alisema taifa hili liko makini katika kuvumbua bidhaa mseto, kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii wanaozuru nchini.

Akiwa ameandamana na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, Miano alizindua rasmi vivutio kadhaa vya utalii, ikiwa ni pamoja na maonyesho ya utamaduni, michezo pamoja na shughuli za matibabu miongoni mwa vivutio vingine.

“Utalii wa nyumbani unasalia kuwa muhimu katika ajenda ya utalii ya taifa hili. Tunapojizatiti kuongeza idadi ya watalii wanaozuru taifa hili hadi milioni tano katika muda wa miaka kadhaa ijayo, macho yetu sasa yanaangazia kuimarisha utalii wa hapa nchini,” alisema Waziri Miano.

Mashindano ya uendeshaji baiskeli yaliyozinduliwa Nyahururu, yanatarajiwa kupitia katika kaunti zingine tano katika muda wa siku tano.

Kulingana na Wizara hiyo, mashindano hayo yatazinduliwa katika sehemu zingine za nchi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *