Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga leo Jumatatu alipeleka kampeni zake za kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC, nchini Zimbabwe.
Akiwa mjini Harare, Raila alikutana na Rais wa nchi hiyo Emmerson Mnangagwa,
“Imekuwa furaha yangu kumwelezea Rais Mnangagwa maono yangu ya Afrika na kujadili ugombea wangu wa uenyekiti wa AUC,” alisema Raila kupitia mtandao wake wa X.
Raila ameimarisha kampeni zake za kugombea uenyekiti wa AUC na amekuwa akitembelea viongozi mbalimbali wa bara la Afrika kutafuta uungwaji mkono.
Siku chache zilizopita, aliitembelea Mauritius na kukutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Dkt. Navinchandra Ramgoolam.
Ramgoolam ameahidi kumuunga mkono Raila kumrithi Moussa Faki ambaye muhula wake unakaribia kumalizika.
Uchaguzi wa uenyekiti wa AUC umepangwa kufanyika mwezi ujao.
Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Mahamoud Ali Youssouf ambaye pia anapigiwa upatu kushinda wadhifa huo.
Mwingine aliye kwenye kinyang’anyiro hicho ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar Richard Randriamandrato.