Timu tano zafuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Dismas Otuke
2 Min Read

Timu tano zimejikatia tiketi kwa robo fainali ya kipute cha Ligi ya Mabingwa barani Afrika CAF, baada ya kumalizika kwa mechi za raundi ya tano mwishoni mwa juma lililopita.

Vilabu vilivyofuzu kwa kwota fainali ni FAR Rabat ya Moroko kutoka kundi B, Orlando Pirates ya Afrika Kusini, na Al Ahly ya Misri kutoka kundi C, Esperance ya Tunisia na Pyramids ya Misri zote za kundi D.

Katika mechi za kundi A, Al Hilal Omdurman ya Sudan ingali kuongoza kwa pointi 10, licha ya kushindwa nyumbani bao moja bila na Yanga ya Tanzania.

MC Alger ya Algeria ni ya pili kundini kwa alama nane kufuatia ushindi wa goli moja bila dhidi ya TP Mazembe wanaoshika nanga kwa pointi mbili.

Kundini B, FAR Rabat ya Morocco waliambulia sare ya bao moja dhidi ya Raja Casablanca, wanajeshi Rabat wakiongoza kwa alama 9, moja zaidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini waliowashinda Maniema ya Congo magoli 2-1.

Pirates wanaongoza kundi C kwa pointi 11 baada ya kuwabwaga CR Belouizdad ya Algeria mabao 2-1, wakifuatwa na mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri kwa alama 10 kufuatia ushindi wa 3-1 ugenini dhidi ya Stade d’Abidjan ya Mali.

Esperance ya Tunisia inaongoza kundi D kwa alama 10, kufuatia ushindi wa bao  moja kwa bila ugenini kwa Djoliba ya Mali, wakifuatwa na Pyramids ya Misri kwa pointi sawa baada ya ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya wenyeji Sagrada ya Angola.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *