Miito imetolewa ya fidia kwa familia za watu watatu waliofariki katika ajali ya ndege katika eneo la Kwa Chocha karibu na uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Malindi katika Kaunti ya Kilifi.
Watu watatu, wakiwemo waendesha pikipiki wawili na abiria mmoja kutoka kata ya Ganda walikuwa wakielekea mjini Malindi wakati ndege ya Cessna 174 iliwaangukia.
Watu watatu waliokuwa kwenye ndege hiyo walinusurika na majeraha madogo.
Huzuni ilitanda nyumbani kwa Felix Khamisi wa umri wa miaka 36, mmoja wa wahasiriwa wa ajali, ambaye ameacha mjane wa umri wa miaka 26 na watoto wawili wa umri wa miaka saba na mwaka mmoja unusu.
Alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa chama cha akiba na mikopo cha waendeshaji boda boda wa Ganda kilichoanzishwa kwa usaidizi wa mwakilishi wa wadi ya Ganda, Oscar Wanje na ina wanachama 300.
Wanje aliiomba Mamlaka ya Usafiri wa Angani nchini Kenya (KCAA) kuanzisha mipango ya fidia kwa familia za wahanga wa ajali hiyo.
Alitoa wito pia kwa serikali kutekeleza mipango ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Malindi, akisema kwamba njia fupi ya uwanja wa ndege inaweza kuwa chanzo cha ajali hiyo kwani ndege iliyoanguka ilikuwa imetoka tu katika uwanja huo na ilikuwa inaelekea Uwanja wa Ndege wa Wilson jijini Nairobi.
“Nilipopata habari za kifo chake, nilianza kufuatilia mchakato wa fidia kwa wahanga watatu wa ajali hiyo na ninaahidi kuwa nitaakikisha fidia inatolewa,” alisema Wanje.
“Tumekuwa tukiomba serikali itekeleze upanuzi wa uwanja huo wa ndege kwa miongo kadhaa na naomba ajali hii iwe ya mwisho na iwe fundisho kwa serikali kwa sababu kesho ndege kubwa inaweza kusababisha ajali hapa na kuleta janga kubwa zaidi. Njia ni fupi sana hata ndege ndogo ya Jambojet inapata shida kutua,” aliongeza.
Loyce Neema Reuben, mke wa marehemu Khamisi, alisema aliguswa sana na kifo cha mumewe akielezea kuwa amebaki mjane akiwa na umri mdogo wa miaka 26.
“Watoto wangu wananiuliza baba yao yuko wapi na mimi najiuliza nitawaambia nini. Inaniuma sana kwa sababu sijui watakula nini na watafundishwa vipi kwa sababu mimi ni mke nyumbani na alikuwa anapanga kunifungulia biashara ndogo,” alisema na kuongeza kwamba “Nina maumivu na kama serikali ingeweza kuchukua majukumu ya kuwasomesha watoto, nitaishukuru.”
Lucas Mwambogo Ngumbao, mjomba wa marehemu, alisema walishirikiana na mamlaka kufanya uchunguzi wa maiti ya marehemu na ripoti ilionyesha kuwa aliuawa na ndege.
“Ripoti ya uchunguzi wa maiti tuliyopatiwa ilionyesha kwamba sehemu za ndege zilimpiga kichwani na katika mbavu na kuathiri moyo, na abiria wa kike aliguswa na sehemu nyingine ya ndege ambayo ilimkata kichwa,” alisema.
Naibu chifu wa kata ya Ganda, Ann Ziro, alitoa tahadhari kwa waendesha pikipiki wanaopanga kukusanya pesa kutoka kwa wananchi kwa kufunga barabara waache na wamtafute ili waweze kukusanya pesa kwa njia iliyopangwa.
“Tuko katika hali ya majonzi lakini nataka kuhimiza vijana wetu wa boda boda kutafuta msaada wangu wanapotaka kuchangisha pesa kwa rafiki yao aliyekufa kwa sababu mara nyingi huwa wanafunga barabara na kuzuia usafiri kabla ya kushurutisha watu kutoa pesa,” alisema.