Makundi ya zimamoto yajitahidi kuzima moto Los Angeles

Moto huo uliendelea kwa siku ya sita mfululizo Jumapili na kuharibu kabisa eneo kubwa la makazi, maafisa wakiripoti kwamba watu wapatao 16 hawajulikani waliko.

Marion Bosire
2 Min Read

Makundi ya wahudumu wa kuzima moto yanajitaidi kuzima moto huko Los Angeles nchini Marekani kabla ya kurejea kwa upepo mkali, huku vifo vikifikia 24.

Moto huo uliendelea kwa siku ya sita mfululizo Jumapili na kuharibu kabisa eneo kubwa la makazi, maafisa wakiripoti kwamba watu wapatao 16 hawajulikani waliko.

Wengine elfu 100, wamelazimika kuhama makazi yao huku nyumba elfu 12 zikiharibiwa.

Msimamizi wa jimbo la Los Angeles, Lindsey Horvath alisema Jumapili kwamba jimbo hilo lilishuhudia usiku mwingine wa shida na majonzi.

Alisema pia kwamba vifo hivyo 24 vinajumuisha vinane vya moto wa eneo la Palisades ambalo liko katika eneo la magharibi la jiji la Los Angeles.

Wengine 16 walifariki katika moto wa Eaton huko foothills mashariki mwa Los Angeles.

Hasara iliyotokana na visa hivyo vya moto kufikia sasa inakisiwa kuwa ya dola bilioni 135 hadi bilioni 150.

Gavana wa California Gavin Newsom aliambia shirika la habari la NBC kwamba visa hivyo vya moto huenda vikawa mkasa mbaya zaidi wa kiasili katika historia ya Marekani.

Katika kusaidia kuharakisha juhudi za kujenga upya eneo hilo katika siku zijazo, Gavana huyo alitia saini agizo kuu, linalosimamisha kwa muda kanuni za mazingira kwa makazi na biashara zilizoharibiwa.

Jumapili wazimamoto wanaotumia ndege walimimina maji waliyochota kutoka kwa bahari ya Pacific pamoja na vitu vingine vya kuzima moto katika eneo linalochomeka huku walio ardhini wakitumia mabomba.

Moto huo umechoma eneo la ekari elfu 23,713 na kiwango cha moto uliozimwa kwa mafanikio kikiwa asilimia 11 pekee.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *