Rais William Ruto ameteua jopo la watu 42 ambalo limekabidhiwa jukumu la kuchunguza visa vya dhuluma za kijinsia nchini ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanawake na kupendekeza namna ya kuvikabili.
Awali, Rais Ruto aliashiria kuwa atabuni jopo hilo kufuatia kuongezeka kwa mauaji ya wanawake yaliyoshuhudiwa nchini mwaka jana.
Jopo hilo litaongozwa na aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu Dkt. Nancy Baraza ambaye kwa sasa ni Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Wanachama wa jopo hilo wanajumuisha Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanawake Mawakili nchini, FIDA Ann Ireri, mwanasheria na mhadhiri Dkt. Linda Musumba, Dkt. Ruth Aura Odhiambo ambaye pia ni mwanasheria na Dkt. Wangu Kanja.
Wanachama wengine ni mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini, LSK Faith Odhiambo, Dkt. Bashir Isaak, Dkt. Mercy Karanja, Dkt. Purity Ngina na Dkt. Sam Thenya miongoni mwa wengine.
Majina ya wote hao yamechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali na jopo hilo lina muda wa miezi mitatu kuchunguza kinachosababisha visa vya dhuluma za kijinsia kuongezeka nchini na kupendekeza njia bora za kukabiliana navyo.
Jopo hilo litaendeshea shughuli zake kwenye ofisi za Wizara ya Usalama Utaifa.