Maafisa wa kliniki wametishia kugoma kuanzia Januari 20, 2025 ikiwa serikali haitaangazia malalamshi yao.
Miongoni mwa malalamishi hayo ni kile Katibu Mkuu wa Chama cha Maafisa wa Kliniki nchini (KUCO) George Gibore anasema ni hatua ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kuwabagua wanachama wake.
“Chama cha Maafisa wa Kliniki kimetambua kwa masikitiko ubaguzi unaofanywa na Mamlaka ya Afya ya Jamii ambayo kimsingi imewazuia maafisa wote wa kliniki kutoa huduma kupitia SHA,” amelalama Gibore kwenye ilani ya siku 14 ya kufanya mgomo ikiwa matakwa yao yatatua kwa sikio la kufa.
“Ubaguzi na uzuiaji huu umesababishwa na ukataaji wa wazi, usiokuwa halali na usiokuwa na mantiki wa SHA kutambua hospitali na maafisa waliosajiliwa na kupewa leseni na Baraza la Maafisa wa Kliniki.”
KUCO pia kimelalamikia vikali hatua ya serikali kukiuka makubaliano ya kurejea kazini yaliyofikiwa mwaka jana na kusitisha mgomo wa maafisa hao uliokuwa umedumu miezi mitatu.
Makubaliano hayo yalifikiwa kati ya KUCO, Wzara ya Afya na serikali za kaunti.
“Inasikitisha kwamba licha ya juhudi za chama kufuatilia na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano haya, waajiri hasa serikali za kaunti wanaendelea kukaidi.”
KUCO sasa kimetoa ilani ya siku 14 ya mgomo kikitaka matakwa yake yote kushughulikiwa la sivyo wanachama wake waanze mgomo kuanzia usiku wa manane, Januari 19, 2025.
Matakwa hayo ni pamoja na kupandishwa vyeo kwa maafisa wa kliniki kama ilivyokubaliwa kwenye makubaliano ya kurejea kazini, kupatiwa bima ya afya na ubadilishaji wa mikataba ya muda mfupi ya utenda kazi kuwa ya kudumu.
Aidha kinataka SHA kurejesha mara moja haki za kuidhinisha huduma za matibabu kwa maafisa wa kliniki wakiwemo wataalam.