Wawili wakamatwa Juja kwa ulanguzi wa bangi

Martin Mwanje
1 Min Read
Afisa wa NACADA Nicholas Kosgey wakati wa opereseheni iliyofanyika mjini Juja na washukiwa wawili wa ulanguzi wa bangi kukamatwa

Watu wawili wamekamatwa katika mji wa Juja, kaunti ya Kiambu kwa kushukiwa kuhusika katika ulanguzi wa bangi. 

Wawili hao walikamatwa jana Alhamisi alasiri katika msako uliofanywa na Mamlaka ya Taifa ya Kupambana na Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA).

NACADA ilishirikiana na Huduma ya Taifa ya Polisi, maafisa wa utawala wa serikali kuu na timu ya uratibu wa kaunti ya Kiambu katika kutekeleza operesheni hiyo baada ya kupashwa habari na raia juu ya ulanguzi huo.

Operesheni hiyo nayo ilifanywa kufuatia wiki kadhaa za ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.

Washukiwa walikamatwa katika nyumba ya makazi mjini Juja na wanaaminika kuwauzia wakazi bangi hiyo.

Wakati wa msako huo, timu hiyo ilipata nyenzo kadhaa haramu ikiwa ni pamoja na takriban misokoto 500 ya bangi na vipimo viwili vya dijitali na makasi.

Washukiwa walipelekwa katika kituo cha polisi cha Juja ili maelezo kuwahusu kunakiliwa na kisha kusafirishwa hadi kituo cha polisi cha Muthaiga walikozuiliwa wakisubiri kufikishwa mahakamani leo Ijumaa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa amesisitiza dhamira ya mamlaka hiyo kukabiliana vikali na ulanguzi na matumizi ya mihadarati nchini na kuahidi kuendelea kufanya kazi na asasi zingine za usalama kuhakikisha hilo linaafikiwa.

 

 

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *