Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, amekumbatiwa na Uingereza siku moja baada ya kukosa maelewano na uongozi wa Marekani.
Sasa waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amemkumbatia Zelenskyy na kumhakikishia kuhusu uungwaji mkono wa dhati kutoka kwa nchi yake.
Zelenskyy aliwasili Uingereza Jumamosi ambapo umati wa watu ulimshangilia huku ukifoka maneno ya kumuunga mkono nje ya makazi ya Starmer ambaye alimkumbatia kabla ya kuingia naye ndani.
“Umekaribishwa sana hapa Downing Street na kama ulivyosikia kutoka kwa watu hapo nje, unaungwa mkono kikamilifu kote Uingereza.” Starmer alimhakikishia Zelenskyy.
Zelenskyy naye alishukuru kwa makaribisho mema na usaidizi ambao nchi yake imepata kutoka kwa Uingereza tangu vita vilipozika kwenye nchi yake.
Leo Jumapili, Zelenskyy anatarajiwa kukutana na mfalme wa Uingereza na anafurahia kwa kuwa na mshirika wa kimkakati katika Uingereza.
Katika mkutano wa jana, Uingereza na Ukraine zilitia saini makubaliano ya mkopo wa Yuro bilioni 2.26 wa kusaidia kuinua uwezo wa kujilinda wa Ukraine.
Ukraine inatarajiwa kulipa mkopo huo kwa faida itakayotokana na mauzo ya mali yake.
Kongamano la viongozi wa Uingereza na Zelenskyy linatarajiwa kuandaliwa leo na afisi ya Starmer inasema linalenga kuhakikisha usaidizi wa kupata amani ya kudumu na ya haki nchini Ukraine.
Haya yanajiri baada ya mkutano kati ya Rais huyo wa Ukraine na Rais wa Marekani Donald Trump kuishia pabaya.
Mbele ya wanahabari wa Marekani na wa kimataifa, Trump na naibu wake Vance walimzomea Zelenskyy, wakimlaumu kwa kile walichokitaja kuwa kukosa shukrani.
Walimlaumu pia kwa kukosa kukubaliana na mapendekezo yao ya kukomesha vita na kurejesha amani nchini Ukraine.
Zogo hilo la Ijumaa lilishangaza viongozi wengi wa Uingereza, kwani Zelenskky aliambiwa kwamba hakuwa na chaguo ila kuingia kwenye mkataba na Marekani la sivyo abaki peke yake.
“Utaingia kwenye mkataba nasi au tujiondoe, na tukijiondoa utapambana peke yako na usifikirie kwamba itakuwa rahisi.” Trump alimwambia Zelenskyy.
Trump alikuwa pia amewasiliana na kiongozi wa Urusi, iliyovamia Ukraine miaka mitatu iliyopita na hivyo kuzua vita, akitaka waafikie makubaliano kuhusu Ukraine.