Wizara ya Afya imezindua kampeni ya utoaji chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza wa Polio, kuanzia Februari 21 hadi 25, katika kaunti za Marsabit, Wajir, Garissa na Mandera.
Kupitia kwa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa, katibu katika wizara ya Afya Mary Muthoni, alisema kampeni hiyo inawalenga watoto 176,949 walio chini ya umri wa miaka 11 Marsabit na watoto 651,252 walio chini ya umri wa miaka tano katika kaunti za Wajir, Garissa na Mandera.
Awamu nyingine ya utoaji chanjo imepangwa kutekelezwa mwezi Aprili katika kaunti hizo hizo, ambazo zimetambuliwa kukabiliwa na hatari kubwa ya maambukizi kutokana na idadi ndogo ya wanaopewa chanjo na shughuli za mpakani.
Katibu Muthoni alisema hatua ya kampeni hiyo inajiri baada ya ugonjwa wa Polio kuthibitishwa kuzuka nchini Ethiopia katika eneo la Moyale Oktoba mwaka 2024, kilomita 15 kutoka mpaka wa Kenya.
“Ni muhimu kudokeza kuwa katika kila kisa kilichothibitishwa, kuna zaidi ya visa 200 ambavyo havijathibitishwa na hivyo ipo haja ya kuchukua hatua kuzuia maambukizi,” alisema katibu Muthoni.
Alitoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanachanjwa hata ikiwa walichanjwa hapo awali, ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
“Tunahakikishia umma kwamba chanjo inayotolewa ni salama na imefanyiwa uchunguzi wa kina. Kupokea chanjo mara zaidi ya moja hakuna madhara kwa mtoto wako, lakini kunaongeza kinga dhidi ya magonjwa,” aliongeza katibu huyo.
Alitoa wito kwa wananchi kuripoti visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya Polio katika kituo cha afya kilicho karibu au kupitia nambari za simu za wizara ya Afya 719, 0729 471414, au 0732 353535.