Vijana kutoka kaunti za Pwani wamekumbatia Mswada wa Vijana 2024 uliopendekezwa na serikali huku ukusanyaji wa maoni kutoka kwa umma ukianza rasmi mjini Kilifi.
Katika mkutano wa kushirikisha umma uliohudhuriwa na vijana kutoka kaunti za Mombasa, Kilifi, Kwale, Lamu, na Taita Taveta, vijana hao walielezea furaha yao kwa kuhusishwa katika mchakato wa kutunga sheria hiyo, wakisema mswada huo umetilia maanani matakwa yao barabara na hivyo kuwapa matumaini mapya.
Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa kwenye mkutano huo ni kuanzishwa kwa mfuko wa kukuza ubunifu wa vijana, kubaini wazi dhuluma za kijinsia zitakazowekwa kwenye sera za kulinda vijana, kuongeza rasilimali za kusaidia vijana kuinuka kiuchumi pamoja na kuzingatiwa kwa maslahi ya vijana walio na ulemavu.
Baadhi ya vijana pia walilalamika kuwa nafasi za kuendesha mswada huo zimepewa wazee, kinyume cha matarajio yao wakieleza wasiwasi kwamba huenda hata nafasi za uongozi katika utekelezaji wa sheria hizo pia zikatolewa kwa wazee, hali ambayo walisema itawanyima vijana nafasi ya kufaidi matunda ya sheria hizo.
Vijana hao waliitaka serikali kuhakikisha mapendekezo yao yanajumuishwa kikamilifu katika mswada huo ili kuuboresha na kuhakikisha unakidhi mahitaji ya vijana humu nchini.