Serikali ya kaunti ya Nandi imeimarisha vita dhidi ya ugonjwa wa malaria baada ya kuzindua rasmi kampeni ya ugavi wa vyandarua kwa wakazi katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo.
Kampeni hiyo ilizinduliwa na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Dkt. Yulita Cheruiyot ambaye pia ni kaimu Waziri wa Afya na Usafi.
Hususan, kampeni hiyo inalenga kuwakinga wakazi wa kaunti ndogo za Tindiret na Aldai dhidi ya ugonjwa wa malaria. Kaunti ndogo hizo mbili zimeathiriwa mno na makali ya ugonjwa huo katika kaunti ya Nandi.
“Afya ni kipaumbele chetu. Wakati tukizindua kampeni ya kupatiana vyandarua kote katika kaunti hii, hebu tuzitumie kukabiliana na ugonjwa wa malaria, moja ya magonjwa yanayosababisha vifo vingi nchini,” alishauri Dkt. Cheruiyot.
Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika katika zahanati ya Kobujoi Forest.
Kampeni hiyo inafanywa kwa ushirikiano na serikali ya kaunti, serikali kuu na washikadau wengine wakuu katika vita dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Kulingana na Dkt. Cheruiyot, kampeni hiyo inatoa kipaumbele kwa makundi yaliyopo hatarini ikiwa ni pamoja na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, kina mama wajawazito na familia za kipato cha chini.