Mwanawe aliyekuwa Rais wa Zambia Edgar Lungu alikamatwa na maafisa wa usalama nchini humo jana Jumanne Februari 11, 2025 kwa kosa la kujipatia pesa kwa njia zisizostahili.
Binti huyo kwa jina Tasila Lungu, ambaye ni mbunge wa eneo la Chawama alitiwa mbaroni baada ya kurejea kutoka Marekani kulingana na tume ya kukabiliana na dawa za kulevya nchini humo.
Analaumiwa kwa kumiliki mali inayokisiwa kununuliwa kwa kutumia pesa za uhalifu na visa vya utakatishaji kulingana na msemaji wa tume hiyo ya kupambana na dawa za kulevya Allan Tamba.
Tasila wa umri wa miaka 41 anadaiwa kumiliki shamba kubwa la thamani ya Kwacha milioni 8.8 sawa na milioni 40 za Kenya Mashariki mwa Zambia kati ya mwaka 2015 na 2022, ambapo alitekeleza kilimo na ufugaji.
Babake Rais Edgar Lungu alikuwa mamlakani kati ya mwaka 2015 na 2021 na familia hiyo imekuwa ikikabiliwa na polisi mara kadhaa.
Mwezi Mei mwaka 2024, Tasila alikamatwa pamoja na mamake na dadake kwa madai ya ulaghai, madai ambayo familia hiyo ilipuuzilia mbali na kuyataja kuwa kisasi cha kisiasa.
Mwana wa kiume wa Rais Lungu aitwaye Dalitso naye anakabiliwa na madai ya ufisadi huku polisi wakivamia makazi ya familia hiyo mwaka 2023 kwa madai kwamba mkewe Lungu alikuwa ameiba magari.
Lungu aliachia uongozi wa taifa hilo mwaka 2021 baada ya kiongozi wa muda wa upinzani Hakainde Hichilema kuibuka mshindi katika uchaguzi kwa kura nyingi.
Rais Lungu ameonyesha nia ya kuwania Urais katika uchaguzi wa mwaka ujao.