Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani unaonekana kubatilisha uamuzi wa awali wa kukomesha matumizi ya mabilioni ya dola za serikali kwa misaada.
Haya yanafuatia vikwazo vya kisheria na upinzani mkali lakini maafisa wa serikali wanashikilia kwamba wanapanga kukata ufadhili wa shughuli anazopinga Trump.
Mawasiliano ya kubatilisha uamuzi huo yalitolewa Jumatatu jioni, saa za Marekani, ambapo afisi ya bajeti ya Ikulu ya nchi hiyo, iliambia mashirika ya serikali kwamba inabatili mawasiliano ya awali yaliyoagiza kukomeshwa kwa malipo ya ruzuku na mikopo.
Hatua hiyo ilijiri muda mfupi kabla ya kusikilizwa kwa kesi iliyowasilishwa na mawakili wa chama cha Democratic ya kujaribu kufutilia mbali agizo la kukomesha misaada.
Afisa mmoja wa ikulu anataja hatua ya kubatilisha uamuzi huo kuwa namna ya kukabiliana haraka na changamoto za kisheria.
Jaji John McConnell, hata hivyo, alisikiliza kesi hiyo ambapo alisema kwamba anaegemea sana upande wa kutoa agizo la kusitisha utekelezaji wa agizo la kukomesha misaada ingawa hakufanya hivyo mara moja.
Katika kikao cha mahakama kilichoandaliwa kwa njia ya mtandao kutoka Providence, Rhode Island, McConnell aliyeteuliwa na Rais Barack Obama, alisema kwamba majimbo kadhaa yamemshawishi kuhusu athari za agizo hilo.
Yanahisi kwamba agizo hilo huenda likatekelezwa baadaye kulingana na matamshi ya mkuu wa mawasiliano wa Rais Trump.
Serikali inasema kukomeshwa kwa matumizi ya fedha kwa ajili ya misaada kulilenga kuipa muda wa kuhakiki na kukomesha ufadhili wa mipango ambayo Trump anataka kukomesha tangu aliporejea mamlakani.
Mipango hiyo inajumuisha juhudi za kuhimiza ujumuishaji wa utofauti, nishati safi na misaada kwa mataifa mengine.
Agizo hilo lilikuwa tayari limesimamishwa kwa muda na jaji mwingine jijini Washington, ambaye anasikiliza kesi iliyowasilishwa na makundi mbalimbali ya wanaharakati.