Chama cha Jubilee kitamuunga mkono Waziri wa zamani wa Usalama wa Kitaifa Dkt. Fred Matiang’i kugombea urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa chama hicho ambaye pia mbunge wa zamani wa eneo bunge la Ndaragwa Jeremiah Kioni.
Kulingana na Kioni, Dkt. Matiang’i ana uwezo wa kuleta mabadiliko nchini katika muda mfupi ikiwa atafanikiwa kushinda urais.
“Tunamtaka mtu anayeweza kuirejesha nchi kwenye njia sahihi katika kipindi kifupi iwezekanavyo,” alisema Kioni wakati akiwahutubia wanahabari huko Nyandarua.
Aliongeza kuwa ikizingatiwa alihudumu kama Waziri kwa kipindi cha miaka 10 katika utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Dkt. Matiang’i ana tajiriba inayohitajika kufufua miradi iliyokwama na kufufua mipango kama vile Edu-Afya, maono ya mwaka 2030 na pia kuhakikisha ujenzi wa mabwawa uliokwama unarejelewa.
Maoni ya Kioni yanakuja wakati ambapo muungano mpyawa kisiasa umebuniwa ukiwaleta pamoja Naibu Rais wa zamani Rigathi Gachagua, kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia amewahi kuhudumu kama Makamu wa Rais na kiongozi wa chama cha DAP-K ambaye pia ni Waziri wa zamani wa Ulinzi Eugene Wamalwa.
Seneta wa kaunti ya Kisii Richard Onyonka na Seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malalah ni wanachama wa muungano huo ambao utapewa jina baadaye.
Onyonka ameashiria kuwa eneo la Kisii linamuunga mkono Dkt. Matiang’i kumenyana na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao.