Kenya leo Jumatatu, imejiunga na ulimwengu kuadhimisha kampeni ya siku 16 za utoaji uhamasisho na kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake.
Kwa mara ya kwanza, kampeni hiyo iliadhimishwa huku kukiwa na ongezeko la visa vya mauaji ya wanawake na wasichana hapa nchini, hali ambayo imesababisha serikali kuchukua hatua hiyo.
Kampeni hiyo inajiri huku ripoti ya Umoja wa Mataifa ikifichua kwamba wanawake elfu 85 na wasichana waliuawa maksudi mwaka 2023 duniani.
Aidha ripoti hiyo inafichua kwamba asilimia 60 ya mauaji yote ya wanawake yalitekelezwa na wapenzi au jamaa wawaathiriwa.
Rais William Ruto amekashifu vikali mauaji hayo na kutoa wito wa kushitakiwa kwa wahusika, huku akiahidi kujitolea kwa serikali kuunga mkono sera ambazo zitakomesha uovu huo, kwa kutengea mradi huoshilingi Milioni 100 unaonuiwa kukomesha visa vya mauaji wa wanawake kote nchini.
Kampeni hiyo ya kila mwaka inayoanza Novemba 25 ambayo ni siku ya kimataifa ya kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake, hadi Disemba 10 ambayo ni siku ya haki za binadamu, inaambatana na kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni kuungana kukomesha dhuluma dhidi ya wanawake kwa mujibu wa maazimio ya Beijing.