Msafara wa malori 109 ya misaada ya Umoja wa Mataifa yaliyokuwa yamebeba chakula yaliporwa kwa nguvu huko Gaza siku ya Jumamosi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) linasema.
Malori 97 kati ya hayo madereva wake walilazimishwa kwa mtutu wa bunduki kushusha misaada hiyo baada ya kupita katika kivuko cha Kerem Shalom kinachodhibitiwa na Israel, kusini mwa Gaza.
Walioshuhudia walisema msafara huo ulishambuliwa na watu waliojifunika nyuso zao na kurusha maguruneti.
Mkuu wa Unrwa, Philippe Lazzarini hakuwatambua wahusika, lakini anasema “kuporomoka kwa utulivu” huko Gaza kunamaanisha “kuwa kuna mazingira yasiyowezekana kufanya kazi.”
Bila uingiliaji kati wa haraka, uhaba mkubwa wa chakula unatarajiwa kuwa mbaya zaidi kwa watu milioni mbili ambao hutegemea misaada ya kibinadamu, kulingana na Unrwa.
Tathmini iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilionya mapema mwezi huu kwamba kuna “uwezekano mkubwa kwamba balaa la njaa linajongea katika maeneo ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.”
Uporaji wa Jumamosi uliripotiwa kwa mara ya kwanza na shirika la habari la Reuters, ambalo lilimnukuu afisa wa Unrwa huko Gaza.