Willy Paul amwomba Bahati msamaha

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki Willy Paul amemwomba mwanamuziki mwenza Kevin Bahati msamaha kupitia akaunti yake ya Instagram.

Alichapisha picha ya Bahati na familia yake na kuandika, “Nikitazama nyuma kuhusu uzoefu na ndugu yangu, ninatambua kwamba nilivuka mipaka katika matukio kadhaa.”

Willy aliendelea kukiri kwamba anatambua sana familia hasa watoto na kwamba vitendo vyake havikukusudiwa kusababisha yeyote madhara lakini anajua vilieleweka hivyo.

“Ninaomba msamaha kwa dhati kutoka kwa Diana na watoto kwa mgogoro uliojiri.” alimalizia Paul huku akikiri mapenzi aliyonayo kwa familia hiyo ya Bahati.

Katika chapisho jingine, Willy Paul aliandika, “Ndugu yangu mpendwa Bahati tumetoka mbali. Tangu nilipokupa makao hadi uliponishauri kuhusu maisha.”

Aliandika maneno hayo chini ya picha yao ya zamani akisema kwamba kuunganishwa kwao tena ni muhimu sana kwake.

“Shetani karibu ashinde lakini kama kawaida Mungu hutangulia. Sina jingine ila mapenzi kwako ndugu yangu.” Alimalizia Paul.

Bahati kwa upande wake alikubali ombi hilo la msamaha akimwambia Willy Paul kwamba wametoka mbali na wamepambana na changamoto kadhaa ukiwemo uchochole katika mtaa wa mabanda wa Mathare.

Alikubali kwamba wamefanya makosa mbali mbali katika safari yao ya maisha na la muhimu ni kurekebisha kwani Mungu ni Mungu wa nafasi ya pili.

“Zaidi ya yote hakuna kosa linalozidi undugu wetu.” alimalizia Bahati.

Inasubiriwa kuona jinsi wawili hao wataendelea hasa baada ya ushindani na upinzani wa muda mrefu kati yao.

Wakati mmoja Willy Paul alitamka maneno yaliyomkera Diana Bahati kiasi cha kumfikisha mahakamani.

Website |  + posts
Share This Article