Leo ndiyo siku ya mwisho ya awamu ya mwaka huu ya tamasha maarufu la Nyege Nyege nchini Uganda.
Awamu ya mwaka huu iling’oa nanga tarehe 14 na inakamilika leo tarehe 17 mwezi huu wa Novemba mwaka 2024.
Wahusika wote wa tamasha hilo wamelazimika kuvumilia hali ya anga inayobadilika badilika hasa ikizingatiwa kwamba ni msimu wa mvua.
Mvua hiyo hata hivyo haikuwakatisha tamaa wahudhuriaji wa tamasha hilo walioonekana kutiwa moyo zaidi kuendelea kuburudika.
kando na muziki, vinywaji, vyakula, shughuli za kitamaduni na hata maonyesho ya mitindo ya mavazi, wahudhuriaji wa tamasha hilo mwaka huu walitembezwa katika jiji la Jinja.
Alhamisi Novemba 14, 2024 siku ya kwanza ya tamasha hilo ilishuhudia burudani iliyotolewa na wapiga muziki Dj Tony wa Uganda na Dj Festivalist wa Kenya.
Kwenye siku ya pili, wahudhuriaji walitumbuizwa usiku na mchana na wasanii kutoka nchi mbali mbali kama vile Emannuelle Parrerin wa Ufaransa, Altayeb Sega wa Sudan, Oliva wa Columbia, Uncle Shapps wa Kenya na Aniko wa Nigeria kati ya wengine wengi.
Siku ya tatu jana Jumamosi wasanii kadhaa walijukumika kuwatendea haki wahudhuriaji wakiwemo Titi Bakorta wa DRC, Elijah Kitaka wa Uganda, Big Chipi wa Tanzania kati ya wengine wengi.
Siku ya mwisho leo inatarajiwa pia kuwa na shughuli nyingi tu huku wahudhuriaji kutoka nchi mbali mbali wakianza kuondoka.