Dkt Barasa: Madai ya Maaskofu wa kanisa katoliki kuhusu NHIF yanapotosha

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa afya Debora Barasa.

Serikali imepuuzilia mbali madai yaliyotolewa na maaskofu wa kanisa katoliki, kuhusu deni linalodaiwa iliyokuwa hazina ya taifa ya bima ya afya (NHIF).

Waziri wa afya Dkt. Debora Barasa, amesema NHIF inadaiwa na vituo vya afya jumla ya shilingi bilioni 19, ambazo zimekuwa zikiongezeka kwa muda wa miaka kumi iliyopita.

“Serikali inapinga vikali taarifa ya kupotosha iliyotolewa na maaskofu wa kanisa Katoliki kuhusu fedha inayodaiwa iliyokuwa hazina ya bima ya afya NHIF,” alisema Barasa.

Huku akijibu taarifa iliyotolewa na Baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki siku ya Ijumaa, waziri Barasa alithibitisha kuwa serikali imejitolea kikamilifu kulipa deni hilo, akidokeza kuwa tayari shilingi bilioni 7.58 zimelipwa.

Aidha waziri huyo aliongeza kuwa halmashauri ya afya ya jamii (SHA), imesambaza jumla ya shilingi bilioni 5.05 katika vituo mbali mbali vya afya,ambapo shilingi milioni 938 kati ya hiyo, zikisambazwa katika vituo vya afya vinavyomilikiwa na mashirka ya kidini.

Ni vyema kufahamu kuwa hazina ya NHIF iliingia katika mkataba na vituo 8,886 vya afya, vinvyojumuisha vile vya umma, vya kibinafsi na vinavyomilikiwa na mashirika ya kidini,” aliongeza waziri huyo.

Waziri huyo alihakikishia vituo vya afya kuwa shilingi bilioni 2.5 zilizosalia zitatolewa wiki ijayo.

Dkt. Barasa alisema, “Wizara hii imejitolea kutoa huduma nafuu za afya kwa wote”.

Share This Article