Ruto: Uchumi wa Kenya umeimarika

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto amesema uchumi wa Kenya umeimarika wakati juhudi za kuleta mabadiliko humu nchini zikiendelea. 

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo kiwango cha mfumko wa bei kimeripotiwa kupungua kutoka asilimia 3.60 mwezi Septemba hadi asilimia 2.70 mwezi jana.

Kunao wanaosema hiyo ni mara ya kwanza kwa mfumko wa bei kushuka hadi kiwango hicho.

“Uchumi umeimarika, uzalishaji chakula umeongezeka kwa kiwango kikubwa, gharama ya maisha imepungua mno na Ajenda yote ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu inaendelea vyema,” amesema Ruto.

Aliyasema hayo katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatano alipokutana na wabunge kutoka kaunti za Samburu,Turkana na Kakamega kujadili ajenda ya maendeleo ya serikalini nchini.

Rais Ruto anasema wakati wa mkutano huo, walijadiliana juu ya nyumba za gharama nafuu, vituo vya digitali, uunganishaji umeme, maji na miradi ya unyunyiziaji mashamba maji katika kaunti na maeneo bunge yao husika.

Share This Article