Waziri wa mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na misitu Aden Duale, Leo Alhamisi, amezindua mradi wa shilingi Milioni 620 wa kuhifafhi msitu wa Mlima Elgon katika kaunti za Bungoma na Trans-Nzoia.
Mradi huo wa miaka mitano, umefadhiliwa na 7th cycle of the Global Environment Facility (GEF7), kupitia shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na michango kutoka serikali za kaunti ya Bungoma na Trans-Nzoia.
Akizungumza katika uzinduzi huo katika eneo la Kapsokwony, waziri Duale alisema mradi huo utaimarisha maisha ya wakazi wanaoishi karibu na mlima Elgon, kwa kubuni nafasi za ajira na kuimarisha shughuli za kilimo.
Duale alisema mradi huo ni sehemu ya juhudi za pamoja za wadau wa asasi mbali mbali, kuhifadhi msitu wa Elgon ambao ni mojawepo wa vyanzo vya maji hapa nchini.
Aidha waziri huyo alitangaza kuwa Novemba 7 kila mwaka, itakuwa siku ya kuhifadhi msitu wa Mlima Elgon.
“Washika dau wote washirikiane siku hii kupigia darubini maendeleo na kujitolea kuhifadhi msitu wa Mlima Elgon,” alisema Duale.
“Siku ya Mlima Elgon, iwe siku ya umoja, kuheshimu jukumu letu la pamoja la kulinda mfumo ikolojia,” aliongeza waziri huyo.
Wakati huo huo Duale alitangaza marufuku ya serikali dhidi shughuli za ukulima katika misitu asilia kote nchini, akisema zoezi hilo huhujumu juhudi zinazoendelea za uhifadhi.
“Ninapiga marufuku shughuli zote za ukulima Cheptais na maeneo mengine yenye misitu ya kiasili. Maeneo hayo sharti yalindwe,”alisema waziri Duale.
Wengine waliozungumza katika uzinduzi huo ni pamoja na katibu wa idara ya misitu Gitonga Mugambi, naibu Gavana wa Bungoma Janepher Mbatiany, mbunge wa Kimilili MP Didmus Barasa na afisa mkuu wa misitu Alex Lemarkoko.