Wabunge wakataa pendekezo la kuondoa marufuku ya mikataba ya umeme

Marion Bosire
2 Min Read
Opiyo Wandayi, Waziri wa Nishati

Wabunge wamekataa pendekezo la Wizara ya Nishati la kutaka kwamba agizo lililositisha kuafikiwa kwa mikataba ya ununuzi wa umeme liondolewe.

Viongozi hao wanahisi kwamba hakuna hakikisho la usalama wa kutosha kwa walipa ushuru dhidi ya kunyanyaswa na wawekezaji wa kibinafsi.

Wizara hiyo ilikuwa imeomba bunge kuondoa agizo hilo hasa kwenye mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, ikisisitiza umuhimu wa kuongeza vyanzo vya umeme ili kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka nchini Kenya.

Kulingana na Wizara hiyo, ukuaji unaotarajiwa katika matumizi ya umeme unahitaji vyanzo tofauti, ambapo mitambo ya makaa ya mawe inachukuliwa kuwa nyongeza ya uhakika na nafuu kwa umeme unaozalishwa kutokana na maji.

Viongozi wa kamati muhimu kama za ukaguzi, fedha na nyingine walipinga vikali hatua ya kuondoa agizo la kusitisha mikataba ya ununuzi wa umeme.

Wabunge walisisitiza kwamba wizara ya nishati kwanza itekeleze hatua za kuhakikisha miradi inakuwa na usawa na wala sio ya kufaidi wawekezaji kinyume na matarajio ya umma.

Walikuwa wakizungumza huko Naivasha kwenye mkutano wa viongozi wakuu wa bunge la taifa uliohudhuriwa na waziri wa nishati Opiyo Wandayi, katibu wa idara ya nishati na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Kenya Power Joseph Siror.

Wakiongozwa na mbunge wa Mwala Vincent Musyoka, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya nishati bungeni, wabunge walidhihirisha wasiwasi kuhusu wizara kukosa mipango ya kutosha ya ulinzi.

Musyoka alisema hakuna sababu za kutosha za kuondoa agizo hilo na kwamba bunge kama mwakilishi wa wananchi ni lazima lihusike katika maamuzi yanayohusu mikataba ya ununuzi wa nishati.

Alitaja mabadiliko ya hivi maajuzi ya bei ya umeme akisema kwamba bei iliyoidhinishwa rasmi mwaka 2012 ni shilingi 12 kwa kila kilowati.

Mbunge wa Emuhaya Omboko Milemba alisema kwamba sababu ya kuweka agizo la kusitisha mikataba ya ununuzi wa umeme ni kwamba ilikuwa mibaya na ilikuwa inasababisha wakenya wagharamike zaidi ili kupata umeme.

Milemba alisema wizara ya nishati ni lazima iainishe mikakati ambayo imeweka ili kuhakikisha mikataba kama hiyo hainyanyasi wakenya.

Share This Article