Wabunge wataka majibu kuhusu kupandishwa vyeo kwa walimu

Marion Bosire
3 Min Read
Julius Melly, Mwenyekiti wa kamati ya elimu bungeni

Kamati ya Bunge la taifa kuhusu Elimu imeitaka tume ya kuajiri walimu nchini TSC kushughulikia masuala ya utumishi shuleni, hasa uhaba wa walimu wa Sayansi, Fizikia, Biolojia, Kemia na Hisabati

Haya yanafuatia mkutano ambapo TSC iliwasilisha ripoti ya hali ya uajiri wa walimu elfu 46, na maandalizi ya mpito hadi darasa la 9.

Wakiongozwa na mwenyekiti Julius Melly, wanachama wa kamati hiyo walimsaili mkurugenzi mtendaji wa TSC Nancy Macharia kuhusu uajiri wa walimu, utumishi na kupandishwa vyeo.

Melly alikosoa mbinu za uajiri za tume hiyo, akitoa wito wa kuwepo kwa mfumo wazi wa kupandisha walimu vyeo, hasa katika shule zisizo na rasilimali.

“Kila kaunti ndogo inapaswa kuwa na walimu wa kutosha hasa wa masomo muhimu kama vile sayansi na hisabati” alisema Melly.

Mkurugenzi Mtendaji wa TSC Nancy Machairia alifichua kwamba uajiri wa walimu 46,000, uliolenga kubadilisha masharti ya ajira ya walimu wanagenzi kuwa ya kudumu unaendelea.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, mchakato wa kuajiri ulioanza mapema Oktoba, ulivutia jumla ya maombi 314,000.

Walimu 93,646 walituma maombi ya kuajiriwa katika Shule za Msingi ambazo zilitengewa nafasi elfu 6 pekee, walimu 144,177 wakatuma maombi ya kuajiriwa katika shule za sekondari msingi zilizotengewa nafasi 39,550 pekee huku walimu 76, 294 wakituma maombi ya kuajiriwa katika shule za sekondari zilizotengewa nafasi 450 pekee.

Macharia aliwahakikishia wabunge kwamba TSC ilipokea shilingi bilioni 13.4 kuwezesha mabadiliko ya wahitimu hadi masharti ya kudumu na yenye malipo ya kustaafu kuanzia Januari 2025.

Hata hivyo, wanachama wa Kamati hiyo ya elimu waliibua wasiwasi kuhusu uhaba wa walimu wa Sayansi na Hisabati na ukosefu wa mfumo wazi wa kukuza.

“Inatia wasiwasi kwamba hatuna walimu wa kutosha wa sayansi. Je, nchi inaweza kufanya nini ili kuwatia moyo?” aliuliza Jerusha Momanyi.

Nabii Nabwera alidhihirisha kusikitishwa na hatua ya TSC kukosa sera kuhusu walimu wanaohudumu kama makaimu huku akitaja kujua iwapo Macharia anajua wingi wa walimu wanaohudumu kama makaimu walimu wakuu.

Clive Gesairo alihoji jinsi TSC inawasiliana na walimu kuhusu kupandishwa vyeo na vigezo vinavyotumika.

“Kuna zaidi ya walimu 400,000 waliohitimu, wasio na ajira nchini” Macharia alikiri.

Tume hiyo pia ilieleza utayari wake wa kuingia kwenye gredi ya 9 chini ya mtaala wa CBC, ikibainisha kwamba imeajiri walimu 48,550 katika kipindi cha miaka miwili ya fedha iliyopita.

Kati yao, 39,550 wamehitimu na 9,000 waliajiriwa kwa masharti ya kudumu.

Kwa mujibu wa stakabadhi zilizo mbele ya Kamati hiyo, walimu 8,378 wa shule za msingi walipelekwa katika Shule za Sekondari msingi na hivyo kuongeza idadi ya walimu wa sekondari msingi hadi 56,928.

Wanachama wa kamati hiyo ya elimu waliagiza TSC kutoa taarifa za kina kuhusu idadi ya walimu wasio na ajira na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na uhaba wa watumishi, hasa katika shule zenye mahitaji maalum, ambazo zinaripotiwa kukabiliwa na upungufu wa walimu 5,600.

Share This Article