Wakenya wametakiwa kuweka kando tofauti zao na kudumisha umoja miongoni mwao wakati wakiuasi ukabila.
Akihutubia taifa wakati wa sherehe za Siku ya Mashujaa katika kaunti ya Kwale leo Jumapili, Rais William Ruto amesema kuna haja ya kila Mkenya kuwa mstari wa mbele katika kukuza mshikamano wa kitaifa, na kukabiliana na migawanyiko na ukabila kati yao.
“Hebu tukumbuke kuwa bila umoja, uhuru wetu na mustakabali wetu utakabiliwa na tishio,” Rais alionya Wakenya kwenye hotuba yake.
“Pamoja, hatuwezi tukazuiwa na chochote katika matamanio yetu na hatuwezi tukatishwa na changamoto yoyote.”
Kwa kuiga, kupigania na kutetea madili ya taifa na kanuni za maongozi kila siku, Rais Ruto amesema Wakenya wataweza kufuata nyayo za mashujaa kama vile Mekatilili wa Menza na wengineo waliojitolea kuhakikisha Kenya inasonga mbele kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Ili Kuimarisha uvuvi wa kilindini serikali ya Kenya Kwanza imenunua na kusambaza boti 123 kwa jamii za maeneo ya uvuvi ,huku pia kukiwa na mipangi ya kununua vifaa vingine vya uvuvi wa kina kwa gharama ya shilingi milioni 600.