Visa viwili zaidi vya ugonjwa wa Mpox, vimethibitishwa hapa nchni katika muda wa saa 24 zilizopita, huku idadi jumla ya visa hivyo ikifika 12.
Kupitia kwa taarifa leo Ijumaa, waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa, alisema visa hivyo vimegunduliwa katika kaunti zifuatazo: Nakuru (2), Kajiado (2), Taita Taveta (1), Busia (1), Nairobi (1), Mombasa (1), Makueni (1), Bungoma (1), Kericho (1) na Kilifi ( 1).
Kulingana na waziri huyo, wagonjwa watano walioambukizwa ugonjwa huo wanaendelea kupokea matibabu, huku saba wakithibitishwa kupona ugonjwa huo.
Aidha Barasa alidokeza kuwa hakuna maafa yaliyoripotiwa kutokana na ugonjwa huo hapa nchini, kufikia sasa.
Waziri huyo alibainisha kuwa hadi sasa watu 68 waliotagusana na wagonjwa wa MPOX wametambuliwa, ambapo 60 kati yao, wamekamilisha uzingatiaji masharti yanayohitajika kufuatwa ya siku 21.
Watu wawili waliotagusana na waathiriwa wa ugonjwa huo hata hivyo wamefanyiwa uchunguzi na kupatikana Mpox, huku wengine 6 wakisalia chini ya ufuatiliaji.
Katika saa 24 zilizopita, jumla ya wasafiri 15,269 wamekaguliwa katika Vituo mbalimbali vya Kuingia, na kuongeza idadi jumla ya waliokaguliwa kufikia wasafiri 1,161,622.
Wakati uo huo, waziri Barasa alifichua kuwa hakuna kisa chochote cha ugonjwa wa Marburg (MVD) ambacho kimegunduliwa nchini.
Hata hivyo alisema wizara yake imeongeza juhudi za ufuatiliaji baada ya kupokea tahadhari kutoka kwa shirika la afya duniani kuhusu ugonjwa huo.