Kenya imetangaza kuzinduliwa kwa Kibali cha Usafiri cha Eletroniki kwa Wasafiri wa Safari Ndefu Wanaopitia humu Nchini (eTA).
Tangazo hilo limetolewa na Rais William Ruto leo Jumatano wakati wa uzinduzi rasmi wa maonyesho ya utalii ya Magical Kenya uliofanyika katika Bustani ya Uhuru jijini Nairobi.
Ruto amesema hatua hiyo itawawezesha wasafiri kutoka nje ya uwanja wa ndege na kujionea wenyewe namna Kenya inavyovutia.
“Wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kati ya muda wa kusubiri kabla ya kuendelea na safari zao sasa wataweza kujionea namna Kenya inavyovutia badala ya kukaa katika uwanja wa ndege wakisubiri muda wao wa kuondoka,” amesema Rais.
Wakati huohuo, Ruto amesema Kenya imetekeleza sera ya kutohitaji viza na hivyo kufanya iwe rahisi kwa Wakenya kuwakaribisha watu kutoka kila pembe ya dunia, wakiwemo watalii na wafanyabiashara.
“Kenya inaweza kuwa nyumbani kwako ambako wewe na familia yako inaweza ikajionea maajabu ya Magical Kenya kila siku, wakati huo wote wakati ukiwahudumia wateja mahali popote duniani.”
Rais Ruto alisema anatambua wajibu muhimu unaotekelezwa na sekta ya utalii katika kubuni nafasi za ajira, kuendeleza miundombinu na kuileta nchi hii fedha za kigeni.
Kufikia mwaka 2023, Kenya ilipokea zaidi ya watalii milioni mbili na kuiletea mapato ya shilingi bilioni 352.
Kulingana na Ruto, Kenya inalenga kuwavutia watalii milioni tano kila mwaka kufikia mwaka 2027.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii Rebecca Miano amesema juhudi kabambe zinafanywa ili kutumia sekta ya utalii kuchochea ukuaji uchumi nchini.