Wizara ya Afya yamwomboleza Dkt. Desree Moraa

Rachael Rhobi
2 Min Read

Wizara ya Afya imemwomboleza Desree Moraa ambaye hadi wakati wa kifo chake alikuwa daktari mwanagenzi katika hospitali ya Gatundu Level 5, kaunti ya Kiambu.  

Dkt. Moraa aliripotiwa kujiua baada ya kulazimika kufanya kazi kwa zaidi ya saa 24 bila kupata muda wa mapumziko. Ni hali inayosemekana kumsabibishia Daktari huyo kijana msongo wa mawazo.

Kumekupo pia na madai ya kunyanyaswa kwa madaktari wanagenzi katika hosptali mbalimbali za umma nchini.

“Ni kwa huzuni na masikitiko makubwa tunaomboleza kifo cha ghafla cha Dkt. Desree Moraa, mhudumu wa afya kijana aliyechapa kazi kwa kujitolea na aliyeonyesha kuwa na uwezo mkubwa lakini ambaye maisha yake yamefikia kikomo,” alisema Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa katika taarifa.

“Kifo chake kinatukumbusha masaibu ambayo wengi wanapitia kimyakimya, ikiwa ni pamoja na wahudumu wa afya.”

Dkt. Barasa ameahidi kuwa ili kumuenzi mwenda zake, Wizara ya Afya kwa ushirikiano na serikali za kaunti inatekeleza mpango kabambe wa afya ya akili katika maeneo ya kazi unaowalenga wahudumu wa afya kote nchini.

Lengo ni kuhakikisha kwamba mifumo ya kutoa usaidizi inaimarishwa na kwamba wale wanaokumbana na changamoto hawahisi upweke.

Chama cha Madaktari nchini, KMPDU kimekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya madaktari nchini hasa kuboreshwa kwa mazingira yao ya utendakazi.

Hususan, kimekuwa kikitoa wito wa madakari wanagenzi kulipwa mshahara wa shilingi elfu 206,000 kwa mwezi kama ilivyokuwa mbeleni.

KMPDU ilipinga vikali juhudi za serikali kutaka madaktari wanagenzi kulipwa mshahara wa shilingi elfu 70 kwa mwezi, pendekezo lililotolewa wakati wa enzi ya aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha.

Mahakama inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusiana na utata unaozingira malipo hayo kesho Alhamisi.

 

Rachael Rhobi
+ posts
Share This Article