Meli ya MV Uhuru II kuimarisha biashara Afrika Mashariki

Tom Mathinji
1 Min Read
Meli ya MV Uhuru II yaanza uchukuzi katika ziwa Victoria.

Meli mpya ya MV Uhuru II, iliyojengwa kwa kitita cha shilingi bilioni 2.4, imerejelea safari za uchukuzi kutoka bandari ya Kisumu hadi bandari ya Bell nchini Uganda, huku ikianza majukumu yake rasmi katika ziwa Victoria.

Meli hiyo iliyojengwa na kampuni ya kutengeneza meli ya Kenya, ilikabidhiwa rasmi shirika la reli nchini, ambalo litasimamia shughuli zake katika ziwa hilo.

Shughuli za Meli hiyo zinatarajiwa kuwiana na zile za MV Uhuru I, ambayo ilikarabatiwa mwaka 2019, ili kupiga jeki uchukuzi wa bidhaa katika ziwa hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi meli hiyo kwa wizara ya Uchukuzi, waziri wa barabara na uchukuzi Davis Chirchir, alisema Meli hiyo itafanikisha biashara ya kanda hii na uchukuzi katika ziwa Victoria.

“kuingia rasmi kwa meli ya MV Uhuru II kwa shughuli za uchukuzi ziwa Victoria, ni hatua kubwa katika uimarishaji wa miundomsingi na uchumi wa baharini,” alisema Chirchir.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi Soipan Tuya, alipongeza utengenezaji wa meli hiyo akisema umeiweka Kenya kuwa kitovu cha shughuli za baharini, hususan katika uchukuzi wa majini na utengenezaji wa meli.

Soipan alisema meli hiyo mpya itaimarisha uchukuzi wa biashara, itabuni nafasi za ajira na kuboresha shughuli za uchumi katika ziwa Victoria.

Website |  + posts
Share This Article