Wakenya kupata vitambulisho vya taifa ndani ya siku 10

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika idara ya uhamiaji Julius Bitok katika kaunti ya Machakos.

Wakenya sasa watapokea vitambulisho vya taifa katika muda wa siku 10 baada ya kutuma maombi, kuanzia mwezi Oktoba 2024, kulingana na katibu wa idara ya uhamiaji Julius Bitok.

Hatua hiyo ya  kupunguza muda wa kusubiri, umefanikishwa na upatikanaji wa vifaa vipya katika vituo vya Huduma na afisi za kitaifa za usajili kote nchini.

Vile vile vituo hivyo vya kitaifa vya usajili, vimepokea mashini mpya za uchapishaji, na hivyo kuharakisha mchakato wa utayarishaji vitambulisho.

“Sasa haitachukua zaidi ya siku 10 za kufanya kazi kuanzia wakati wa kutuma maombi, kutoka siku 21 awali kupata kitambulisho. Tunataka wakenya kupata vitambulisho haraka iwezekanavyo,” alisema Bitok wakati wa sherehe za kuadhimisha siku ya kitambulisho duniani, zilizoandaliwa kaunti ya Machakos.

Siku ya kitambulisho duniani huadhimishwa tarehe Septemba 16, kusherehekea utambulisho wa taifa na stakabadhi zingine za utambulisho.

Sherehe za mwaka huu katika kaunti ya Machakos, zilitoa fursa za usajili wa moja kwa moja wa vitambulisho, hati za kuzaliwa, cheti za maadili mema na stakabadhi zingine muhimu.

Kaunti ya Machakos ilichaguliwa kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliohitimu kuchukua vitambulisho, huku vijana 32,000 wakisubiri kusajiliwa.

Share This Article