Dorcas: Vita dhidi ya pombe haramu viimarishwe

Tom Mathinji
1 Min Read

Mke wa Naibu Rais Mchungaji Dorcas Rigathi, ameshikilia haja ya taifa hili kushirikiana kuimarisha vita dhidi ya uraibu wa pombe na utumizi wa mihadarati.

Dorcas alishtumu juhudi zozote zinazolenga kurejesha nyuma hatua zilizopigwa, katika kampeni za kuangamiza uraibu huo.

Aliyasema haya wakati wa maonyesho ya ujuzi wa wanaume 303 waliopokea mafunzo mbali mbali ya kiufundi, katika kaunti ya Nyeri.

“Wengine wameapa kurejesha uraibu wa pombe kwa watoto wetu, huku sisi tukijitahidi kumaliza uraibu huo. Chochote ambacho kinawaangamiza watoto wetu ni cha kishetani. Uangamizaji wa mtoto wa kiume Kupitia pombe, unapaswa kukomeshwa,” alisema Dorcas.

Wanaume hao 303 walipokea mafunzo hayo Kupitia mpango wa kumwezesha mtoto wa kiume unaotekelezwa Mchungaji Dorcas kwa ushirikiano na taasisi ya kiufundi ya Vera kwa muda wa miezi mitatu iliyopita.

“Hii ni safari ya kumwezesha mtoto wa kiume kujitegemea. Nahimiza makanisa na jamii katika eneo hili kuwaajiri hawa vijana iwapo watahitaji huduma zao,” alisema Dorcas.

Share This Article