Mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika bunge la kaunti ya Turkana William Samal Etubon alihudhuria maonyesho ya kila mwaka ya kampuni ya utafiti wa mbegu Kenya seed katika kaunti ya Trans Nzoia.
Waziri wa kilimo Andrew Karanja aliyeongoza maonyesho hayo katika makao makuu ya kaunti ya Trans nzoia alieleza dhamira ya serikali ya kuhakikisha wakulima wanapata mbegu na mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati unaofaa ili kuhakikisha usalama wa chakula humu nchini unaimarishwa.
“Kama serikali hatutaki tena wakulima wetu wahangaike kwa sababu hakuna mbolea tutahakikisha wakulima wamepata mbegu na mbolea iliyodhibitishwa ili kuhakikisha tunapata chakula cha kutosha” alisema karanja.
Mwenyekiti wa kamati ya kilimo katika bunge la kaunti ya Turkana William Samal Etubon naye amesisitiza haja ya wakulima kupatiwa mbegu za kutosha na zilizodhibitishwa kuwa salama ili kuhakikisha usalama wa chakula katika kaunti hiyo inayoshuhudia makali ya kiangazi.
“Mashamba yetu katika kaunti ya Turkana yana uwezo wa kuzalisha vyakula vya kutosha kwa watu wetu ikiwa kama bunge la kaunti ya Turkana tutawalinda wakulima wetu kwa kutunga sheria ambayo itawapa wakulima uwezo wa kupata mbegu na mbolea kwa bei nafuu. Itazuia utegemezi wa chakula cha msaada” Alisema Wiliam.
Mwakilishi huyo wa wadi ya Katilu alipata fursa ya kutangamana na watafiti wa mbegu kutoka kampuni hiyo ya Kenya Seed ambapo walikubaliana kushirikiana katika usambazaji wa mbegu hizo kwa mashamba ya Turkana.
Mwenyekiti huyo amewahakikishia wakulima kuwa watapata mbegu safi na salama zitakazotumika katika mashamba haswa katika ukanda wa mto Turkwel.