Madaktari wanaofanya kazi katika kaunti 11 humu nchini wametoa ilani ya mgomo ya siku 14 kufuatia kucheleweshwa kwa ishahara yao.
Kupitia kwa chama chao KMPDU, madaktari katika kaunti za Lamu, Kakamega, Taita Taveta, Garissa, Meru, Isiolo, Marsabit, Kirinyaga, Samburu, Nakuru na Mandera wametishia kugoma kufuatia kucheleweshwa kwa mishahara ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu.
Chama cha KMPDU kimetoa pia ilani ya siku 14 ya mgomo wa madaktari wa kaunti za Nandi na Mombasa ambao hawakulipwa mishahara ya Machi na Aprili mwaka huu kutokana na mgomo wa wakati huo ilhali mahakama iliagiza walipwe.
Katibu mkuu wa KMPDU Daktari Davji Atellah amelalamikia matokeo ya mkataba wa kurejea kazini uliotiwa saini na serikali za kaunti na ile ya kitaifa.
Anasema walifaa kuanza kupokea malimbikizi ya mishahara ya miaka saba mwezi Julai mwaka huu lakini serikali ya kitaifa haijachukua hatua kufikia sasa.
Pesa hizo kulingana na Atellah zilistahili kutolewa Julai na Agosti ila bado.
Serikali za kaunti zimejitetea kwa kutolipa pesa hizo zikisema kwamba hazijapokea hela kutoka kwa serikali ya kitaifa.
Akizungumza na wanahabari Jumamosi Agosti 24, 2024, Atellah alisema madaktari wana subira lakini haifai kuchukuliwa visivyo.
Alitishia kushtaki serikali kwa kutotii maagizo ya mahakama na kuongeza kusema kwamba wako tayari kugoma tena kuitisha pesa walizoahidiwa.