Hazina ya kitaifa ya utafiti imezindua tuzo za kitaifa za utafiti, kutambua na kufurahia michango ya kipekee ya utafiti na uvumbuzi hapa nchini.
Tuzo hizo za kifahari zilizinduliwa wakati wa sherehe ya ufunguzi ya tamasha za kitaifa kuhusu utafiti za mwaka 2024.
Miongoni mwa wale waliotuzwa ni pamoja na Prof. Mary Abukutsa-Onyango kwa mchango wake wa utafiti katika sayansi ya kilimo hususan kupigia debe mboga za kiasili na mimea, ambao umechangia pakubwa kuimarisha usalama wa chakula na lishe hapa nchini na katika mataifa ya nje.
Dkt. Oscar Omondi Donde alituzwa kwa mchango wake wa kuhakikisha mazingira endelevu hasaa usimamizi wa rasilimali za maji na afya ya mfumo ikolojia. Uongozi wake katika chuo kikuu cha Egerton na mikakati yake ya utafiti yameimarisha utunzaji wa mazingira Barani Afrika.
Christine Wayua Musyimi, alituzwa kwa juhudi zake za ubunifu katika kushughulikia afya ya akili ya jamii na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ya akili katika maeneo duni hapa nchini.
Wakati huo huo mhandisi Aggrey Shitsukane Shisiali alituzwa kwa mchango wake katika uhandisi wa umeme, hususan katika taasisi za mafunzo ya kiufundi (TVET).
Tuzo za mwaka huu pia zilishuhudiwa kuanzishwa kwa tuzo za maisha za utafiti. Watafiti ambao kazi zao zilibadilisha taswira ya utafiti hapa nchini, walituzwa.
Waliopokea tuzo hiyo ni pamoja na Prof. David Musyimi Ndetei kwa kazi yake katika afya ya akili, Prof. Ruth Nduati kwa kuanzisha utafiti kwa afya ya watoto na uzuiaji wa maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto. Prof. Paul Kamau Mbugua pia alipokea tuzo hiyo.